Nahodha
wa Timu ya Baseball ya Kibasila Pius Peter (kulia) akiwaonyesha
waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam jinsi ya mchezo huo
unavyochezwa. Kushoto ni Nahodha wa Timu ya Baseball ya Tigers Mussa
Mbugi.
Nahodha
wa Timu ya Baseball ya Kibasila Pius Peter (wa pili kulia ) akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu Mashindano ya
Kitaifa ya Awamu ya Tatu ya Mchezo wa Baseball yanayotarajia kuanza
Ijumaa ya wiki hii jijini Dar es salaam . Wengine Katibu Mkuu wa Chama
cha Mchezo wa Baseball nchini Alpherio Nchimbi(kushoto) ,Nahodha wa Timu
ya Baseball ya Tigers Mussa Mbugi( wa pili kushoto) na Nahodha wa Timu
ya Baseball ya Giants Douglas Stanslaus.(kulia).
Na Nyakongo Manyama- MAELEZO.
MASHINDANO ya Kitaifa ya Awamu ya Tatu ya Mchezo wa Baseball yanatarajiwa kuanza Ijumaa ya wiki hii jijini Dar es salaam.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Mchezo wa Baseball
nchini Alpherio Nchimbi leo jijini Dar es salaam wakati wa mkutano na
waandishi wa habari.
Amesema kuwa mashindano yatashirikisha timu tisa kutoka Tanzania bara na
Visiwani na yanatarajiwa kufunguliwa na Balozi wa Japani nchini
Tanzania Mhe. Masaharu Yoshida.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo , mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika
katika shule ya Sekondari ya Azania iliyopo jijini Dar es salaam.
Amesema kuwa mashindano hayo yanayojulikana kama 3rd Koshien Tanzania
National Championship yatafanyika kwa muda wa siku tatu kuanza tarehe 11
hadi 13 mwezi huu.
Nchimbi amezitaja timu zitakazoshiriki kuwa ni Shule za Sekondari ya
Azania, Kibasila , Iyunga, Sanya Juu, Londoni , na Mwanza Baseball Club,
Mwanakwerekwe “C” , Tigers na Giants.
Amesema
kuwa mshindano ya mwaka huu yanatarajiwa kusimamiwa na wataalamu kutoka
nchini Japan wakishirikiana na wataalam kutoka nchini katika kutoa
uamuzi na masuala mengine ya kiufundi.
Nchimbi
amesema lengo la mashindano hayo ni kupata timu ya Taifa ya umri wa
chini ya miaka 21 kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kushiriki mashindano
yatakayofanyika Afrika kusini hapo mwezi wa pili(February ) mwakani
(2016).
Kwa
upande wa Nahodha wa Timu ya Giants Douglas Stanslaus ametoa wito kwa
wananchi wajitokeze kwa wingi kwa ajili kuona mashindano hayo na kuwatia
moyo ili waweze kukuza mchezo huo nchini.
Naye
Nahodha kwa timu ya Kibasila Pius Peter amewaomba vijana wengi
kujitokeza kuona na kujifunza jinsi mchezo huo unavyochezwa ili hatimaye
mchezo huo umeweze kuenea sehemu mbalimbali nchini kama fursa ya vijana
kushirikiana na kujenga umoja.
Aidha
Katibu Mkuu wa Katibu wa Chama cha Mchezo wa Baseball nchini Nchimbi
amewaomba wadau mbalimbali kuthamini mchezo wa Baseball kama ilivyo
michezo mingine na kujitokeza kuufadhili ili uweze kukua na kutengeneza
ajira kwa vijana.