Kocha Louis Van Gaal wa Manchester United anaweza kutimka klabuni
hapo mwisho wa msimu huu pamoja na kuwa bado ana mkataba hadi msimu
ujao. Taarifa zilizoandikwa na magazeti mbalimbali nchini England
zinasema hali sio shwari sana kwa future ya kocha Louis Van Gaal ambaye
sasa presha ni kubwa sana kutokana na kutolewa kwa Manchester United
klabu bingwa Ulaya sanjari na mwendo wa kobe katika ligi kuu soka nchini
England.
Swali kubwa ni nani atakae rithi mikoba ya kocha huyu endapo ataondoka klabuni hapo? Alipoteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa msaidizi mwaka 2013 mchezaji wa zamani wa klabu hiyo Ryan Giggs, taa ya kijani ilianza kuwaka kwa mkongwe huyo aliyecheza kwa mafanikio sana chini ya kocha Sir Alex Ferguson.
Habari zinasema kuwa, Ryan Giggs ndiye chaguo la mkurugenzi mtendaji wa klabu hiyo Ed Woodward na kwamba ndiye atakaye kuwa mrithi wa Van Gaal endapo tu mholanzi huyo ataondoka Old Trafford.
Ryan Giggs amekaa na kocha Sir Alex Ferguson huku akishuhudia utawala wa Manchester United barani Ulaya na ligi za nyumbani lakini sasa amekua akiumia hali akiwa msaidizi tangu 2013. Kimya chake kinaweza kuwa cha kisiasa kuwatega United kuhusiana na kupewa nafasi ya ukocha mkuu baada ya Louis Van Gaal.
Lakini kocha wa Bayern Munich Pep Guadiola anaweza kuwa mrithi wa Van Gaal endapo tu Manchester United itaamua kutafuta mwalimu kutoka nje ya Uingereza. Tayari kuna taarifa za chinichini kuhusu nia ya Pep Guadiola kuwa na mahaba na United, huku hadi sasa akiwa hajasema chochote kuhusu mkataba wake.